Moja ya maeneo yanayohangaikiwa sana linapokuja suala la afya ya uzazi ni pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi. Taarifa sahihi ni jambo moja na upatikanaji wake (eneo taarifa inapotolewa) ni jambo jingine kabisa. Mazingira yetu kama taifa linalopambana kuendana na mageuzi mengi ya kidunia kuna haja ya kuwekeza katika upatikanaji rafiki wa taarifa sahihi za afya ya uzazi.
Jamii zetu zimekwisha kurasimisha matumizi ya neno “maeneo rasmi” na yale “yasiyo rasmi” katika mambo mengi. Sijui ni busara ipi unatumika kuweka muktadha huu, ila wahenga waheshimiwe na ya kale yaenziwe. Hata katika masuala ya afya, tukiangazia eneo la afya ya uzazi kiujumla wake, kuna nadharia ya maeneo rasmi ya upatikanaji wa taarifa sahihi na yale maeneo yasiyo rasmi ya upatikanaji wa taarifa sahihi.
Japo dhana ya neno rasmi na sio rasmi inaweza kuwa ni mjengo wa kijamii (social construct) lakini athari zake ni kubwa ikiwa urasimishaji wa maneno haya ndio unaoamua uwekezaji wetu kama jamii katika kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi kwa vijana balehe na vijana kiujumla unakua na uhalisia.
Mathalani, tukisema eneo rasmi hua mara nyingi tunarejea vituo vya afya au vile vituo rasmi (attachments) ambavyo vinatoa huduma rafiki kwa vijana. Maeneo hayo huwa tunaamini ni rasmi na yanatoa taarifa sahihi za afya ya uzazi kwa vijana balehe na vijana kwa ujumla. Familia ni moja ya maeneo rasmi, japo kuna usiri wa kuelimishana, hakuna urafiki, ni vitisho. Na wazazi wengi hawana taarifa sahihi pia. Japo wapo ambao ni hazina ya taarifa sahihi kwa vijana balehe.
Na tukigusia maeneo yasiyo rasmi huwa tunaangazia maeneo kadhaa ambayo hatuna imani na ukweli wa taarifa wanazotoa (hawajafuata vigezo vya ubora wa taarifa), maeneo hayo mara nyingi ni vikundi rika “holela” vya vijana. Na kwakua tumeamini na tumerasimisha kuwa hilo si eneo rasmi la upatikanaji wa taarifa, huwa tunajiaminisha kwamba taarifa nyingi katika makundi haya ya vijana ni “hatarishi” na si salama kwa ustawi wa afya ya vijana balehe.
Uwekezaji wetu katika upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi unaakisi mno namna gani tumerasimisha maeneo hayo mawili. Lakini tujiulize, kwa yaliyo maeneo rasmi mathalani vituo vya afya au maeneo maalumu yanayojikita na utoaji wa huduma rafiki kwa vijana, je ni maeneo rafiki kwa vijana?
Tafiti nyingi katika pembe kadhaa za Afrika zinaonesha ni asilimia ndogo sana ya vijana inapata taarifa sahihi za afya ya uzazi katika maeneo rasmi yanayofanyiwa uwekezaji. Ni uchache huo unatokana na vijana kutokuwa na imani na usiri wa huduma zao wanazopata katika maeneo hayo rasmi. Hii inafanya waone maeneo hayo rasmi si mbadala wa uhuishaji wa afya zao.
Vijana balehe wengi wapo katika taasisi za elimu. Na kwakua elimu yetu ni bure kuanzia msingi hadi sekondari ya upili (kidato cha tano na sita) basi tunaamini maeneo kama haya kuwa kitovu cha wao kupata taarifa sahihi za afya ya uzazi. Je, maeneo hayo rasmi ya kukutanisha vijana yamewezeshwa au yamekubali kuwa kituo cha taarifa sahihi? Jibu sina ila msomaji unaweza kuwa na majibu yako binafsi.
Yawezekana maeneo yasiyo rasmi yakawa yanatoa taarifa sahihi au pia zisizo sahihi. Hii inategemeana na kwa namna gani mshauri anahudumu katika “soko” hilo la taarifa na huduma. Wapo wataalamu wa afya ambao wanatoa taarifa rasmi katika mazingira yasiyo rasmi kwa watu ambao hawajui “haki rasmi” za wao kupata taarifa sahihi za afya ya uzazi.
Pia wapo wahanga wa ukosevu wa taarifa sahihi za afya ya uzazi ambao wamegeuka washauri juu ya namna gani kijana balehe anaweza kutatua changamoto zake zinazohusu afya ya uzazi.
Maeneo yote rasmi na yale yasiyo rasmi ndio yameshikilia mustakabali wa afya ya kijana balehe wa kitanzania. Na kwa umuhimu mkubwa maeneo yote mawili ni muhimu na nyeti sana. Ni namna gani tunafanya tafiti za uwekezaji ndio namna ambayo itamfanya kijana aidha aende eneo rasmi au lisilo rasmi.
Tukiipenda rasmi na kuwekeza huko basi tusiififishe isiyo rasmi na kuibeza kwa nongwa nyingi. Tuijengee uwezo na kuitambua maana ndio kimbilio “bubu” la vijana balehe wengi katika jamii zetu.